RC CHALAMILA ATEMBELEA TRC KITUO CHA MAGUFULI.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe Albert Chalamila leo Disemba 12, 2025 ametembelea na kukagua kituo cha reli ya Kisasa cha Magufuli na kujionea huduma mbalimbali zinazotolewa katika kituo hicho.
RC Chalamila akiwa katika kituo hicho ametembelea maduka ya biashara mbalimbali kisha kupata wasaa wa kuongea na menejimenti ya TRC ikiongozwa na mtendaji mkuu Mhandisi Machibya Masanja ambapo ameweza kuelezwa kwa kina mipango ya shirika hilo.
Aidha RC Chalamila ameihakikishia TRC kuwa Dar es Salaam ni salama sana hivyo shirika hilo na watumiaji wa usafiri huo wajisikie wako salama sana
Vile vile amesema Mkoa uko makini kuilinda miundombinu ya TRC, kwa kushirikiana na wakuu wengine wa mikoa ambao wanapitiwa na SGR kama vile Pwani, Morogoro na Dodoma " mara zote tumekuwa na vikao vya pamoja vya kuweka mikakati ya kulinda miuondombinu hiyo ya SGR" Alisema RC Chalamila.
Sanjari na hilo RC Chalamila ameitaka TRC inapotekeleza miradi iwafanye wananchi au jamii kuwa ni sehemu ya miradi hiyo kwa kuwapatia kazi ndogondogo ikiwemo kufanya usafi na walipwe fedha, kwa kufanya hivyo itasidia sehemu au kijiji ambako mradi unapita jamii kuweza kulinda miundombinu ya reli kwa kuwa itajua mradi huo ni wa kwao.
Pia Mkuu wa Mkoa amesema Mkoa huo unakua kwa kasi sana hali inayopelekea kuwepo kwa changamoto ya foleni hivyo ameitaka TRC kuona namna wanavyoweza kuwa sehemu ya kutatua changamoto hiyo kwa kujenga reli ya kisasa ya mjini ambayo itakuwa inatoa huduma katika Mkoa huo.
Sambamba na hilo RC Chalamila amesisitiza kuharakisha kukamilisha ujenzi wa miundombinu ya reli kuingia bandarini ili kupunguza adha ya malori mengi barabarani, vilevile kuendelea kusimamia kikamilifu mradi huo kwa kuwa unataswira chanya ya ukuaji uchumi wa kitaifa.
Mwisho kwa upande wa Mhandisi Machibya Masanja amekiri kupokea na kufanyia kazi maagizo ya Serikali ambapo amemuhakikishia Mkuu wa Mkoa kuwa shirika hilo liko mbioni kujenga reli za kisasa katika miji mikubwa kwa kuanzia wataanza na Jiji la Dar es Salaam na Dodoma.




Comments
Post a Comment