TCCIA YAPANGA MAGEUZI MAKUBWA: MINJA NA ROSTAM WAZUNGUMZA JUU YA KUINUA BIASHARA NCHINI.
Dar es Salaam — Rais wa Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA), Bw. Vicent Minja, amekutana na mfanyabiashara maarufu na mmiliki wa kampuni mbalimbali nchini, Bw. Rostam Aziz, kwa mazungumzo mahsusi kuhusu fursa za uwekezaji, mustakabali wa sekta ya biashara, na mwelekeo mpya wa chemba katika kukuza uchumi wa Taifa.
Katika mazungumzo hayo, pande zote mbili zimeweka wazi dhamira ya kuijenga TCCIA mpya chemba yenye nguvu, inayosikilizwa, na inayoongoza katika kutengeneza sera za taifa upande wa biashara na uwekezaji.
Bw. Rostam Aziz, akitoa mchango wake, alisisitiza umuhimu wa wafanyabiashara kuunga mkono chemba na kuitambua kama chombo kikuu cha kuimarisha mazingira ya biashara nchini.
“Chemba ni chombo kikubwa kwa ukuaji wa biashara. Inapaswa kupata sapoti kutoka kwa wafanyabiashara na hata kwa Rais wa nchi. Tukijenga Chemba imara, tutaijenga Tanzania yenye uchumi madhubuti. “Let’s start a new chapter” Chemba ichukue nafasi yake katika taifa,” alisema.
Akiendelea, Rostam alisisitiza umuhimu wa kubadili mtazamo kuhusu mchango wa wafanyabiashara wazawa katika maendeleo ya nchi.
“Mimi nilipopitia changamoto, Chemba ilinilinda. Wafanyabiashara wakiona jinsi Chemba inavyotetea maslahi yao, wataelewa umuhimu wake. Ni wakati Watanzania waunge mkono juhudi za wafanyabiashara wazawa badala ya kuwanyooshea vidole,” aliongeza.
Kwa upande wake, Rais wa TCCIA, Bw. Vicent Minja, alieleza kuwa mafanikio ya chemba yanaakisi moja kwa moja mafanikio ya wafanyabiashara wake.
“Chemba ikifanya vizuri, kila mfanyabiashara atanufaika. Tunahitaji kuijenga upya, kuipa nguvu, na kuhakikisha sauti yetu inasikika kwenye majukwaa ya kutengeneza sera. Tukisimama kama mtu mmoja kupitia Chemba, changamoto za kibiashara zitashughulikiwa kwa ufanisi zaidi,” alisema Minja.
Mazungumzo haya yamefungua ukurasa mpya wa ushirikiano kati ya TCCIA na wadau wakubwa wa biashara nchini, huku dhamira kuu ikiwa ni kuijenga chemba imara, jumuishi na yenye uwezo wa kuongoza mageuzi chanya ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.




Comments
Post a Comment