TCRA-CCC Yatakiwa Kuongeza Ushirikiano na Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano.

Na Mwandishi Wetu,

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki (Mb), ameitaka TCRA Consumers Consultative Council (TCRA-CCC) kuimarisha ushirikiano na watumiaji wa huduma za mawasiliano nchini, hususan katika kushughulikia malalamiko na changamoto wanazokabiliana nazo.


Akizungumza leo, tarehe 08 Desemba 2025, jijini Dar es Salaam wakati wa ziara yake ya kikazi katika Baraza hilo, Waziri Kairuki amesema TCRA-CCC lina nafasi muhimu katika kuhakikisha haki na maslahi ya watumiaji wa huduma za mawasiliano yanalindwa kwa ufanisi.


Amesema ni muhimu Baraza hilo kufuatilia kwa ukaribu mchakato wa kupokea na kushughulikia malalamiko ya wananchi, huku likionesha kwa uwazi aina ya malalamiko yaliyokwisha kutatuliwa na yale yanayoendelea kufanyiwa kazi. Ameeleza kuwa ufuatiliaji huo utasaidia kujenga imani ya wananchi na kuongeza uwajibikaji kwa watoa huduma.


“Baraza lijenge uwezo na mifumo imara ya kushughulikia malalamiko. Wananchi wanapaswa kuona hatua zinazochukuliwa na kufahamu namna haki zao zinavyolindwa,” amesema Mhe. Kairuki.


Aidha, Waziri Kairuki ameagiza TCRA-CCC kuongeza ushirikiano na wadau wake mbalimbali, ikiwemo makampuni ya mawasiliano, watumiaji binafsi na makundi maalum ya jamii, ili kuhakikisha changamoto zao zinatolewa kipaumbele na kupatiwa ufumbuzi wa haraka na wa kisheria.


Amesema ushirikiano huo ni muhimu katika kuimarisha uwazi, kuboresha huduma kwa wananchi na kuhakikisha kuwa kero za watumiaji zinatatuliwa bila kucheleweshwa.


Waziri pia amelitaka Baraza kuongeza kasi ya utoaji wa elimu kwa umma kuhusu haki za watumiaji na matumizi sahihi ya huduma za mawasiliano, akibainisha kuwa uelewa mdogo miongoni mwa wananchi mara nyingi husababisha malalamiko yasiyoratibiwa vizuri na matumizi yasiyo sahihi ya huduma hizo.


“Elimu ya kutosha itawasaidia wananchi kufahamu haki zao na wajibu wao. Pia itawasaidia watoa huduma kuboresha uwajibikaji,” amesema.


Akihitimisha ziara hiyo, Waziri Kairuki amesisitiza kuwa TCRA-CCC ni chombo muhimu katika sekta ya mawasiliano, kwa kuwa kinatoa mchango mkubwa katika kulinda haki za wananchi, hususan wale wenye mahitaji maalum, ili kuhakikisha kila mtu ananufaika ipasavyo na huduma za mawasiliano nchini.

Comments

Popular posts from this blog

RC CHALAMILA AWATAKA WENYEVITI NA WATENDAJI KATA NA MITAA DAR KUSIMAMIA ULINZI NA USALAMA.

MAHAFALI YA NANE SHULE YA AWALI NA MSINGI SAI YAFANA, WAZAZI WATAKIWA KULEA WATOTO KATIKA MISINGI YA MAADILI MEMA.