WAJASIRIAMALI DAR WALAANI MACHAFUKO YA OKTOBA 29, WASISITIZA AMANI NA MAENDELEO.


Wajasiriamali wa kada mbalimbali kutoka wilaya zote tano za Mkoa wa Dar es Salaam wamelaani vikali machafuko ya 
Oktoba 29, wakisema yameathiri maisha ya wananchi, biashara, ajira na uchumi wa mkoa pamoja na Taifa.


Wakiwasilisha tamko lao hilo kwa wanahabari  jijini Dar es Salaam kwa niaba ya wajasiriamali wa mkoa huo akiwemo Mohamed S. Mohamed wa Temeke, Hussein Bambe wa Ubungo, Zahra Sadicky wa Kigamboni, Bakari Sufiani Mofi wa Ilala na Sharifu Hassan wa Kinondoni wamesema machafuko hayo yamesababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu ya umma, ikiwemo mabasi ya mwendokasi (BRT), hali iliyowalazimu wananchi kukosa huduma muhimu za usafiri huku watumishi wengi wakipoteza ajira au vyanzo vya kipato.


Wamesema uharibifu huo umeiacha jamii na mzigo mkubwa wa kiuchumi, huku wafanyabiashara wengi wakipoteza mitaji na mali waliyojenga kwa muda mrefu ndani ya kipindi kifupi.


Aidha, wajasiriamali hao wamesema uchomaji wa moto kwenye biashara na taasisi za kazi umesababisha wafanyakazi wengi kukosa ajira, familia kukosa kipato na kuongezeka kwa changamoto za maisha. Vifo na majeruhi vilivyotokana na machafuko hayo vimeongeza majonzi kwa familia na jamii.


Kwa mujibu wa tamko hilo, licha ya kuwepo kwa changamoto na malalamiko halali ya wananchi, hakuna sababu inayoweza kuhalalisha uvunjifu wa amani, uharibifu wa mali za umma na binafsi au kupoteza maisha ya wananchi.


Pia wamesema kuwa tukio la Oktoba 29 limebainisha kuwa vurugu hazina suluhu, uchochezi haujengi na matusi kwa viongozi wa Serikali hayatatui changamoto za wananchi. Pia wamedai kuwa machafuko hayo yamekuwa yakihamasishwa na baadhi ya wanaharakati walioko nje ya nchi pamoja na wanasiasa wanaotumia hasira za wananchi kama mtaji wa kisiasa bila kubeba gharama za matokeo yake.


Kutokana na hali hiyo, wajasiriamali hai wamesema wamechagua amani kama msingi wa kulinda biashara, ajira na ustawi wa Taifa, wakisisitiza matumizi ya mazungumzo, mifumo ya kisheria na ushiriki wa wadau katika kutatua changamoto.


Hata hivyo wajasiriamali hao wamesisitiza kuwa hakuna changamoto inayotatuliwa kwa machafuko au uchochezi, na kwamba amani ndiyo nguzo kuu ya maendeleo na mustakabali wa Taifa.








Comments

Popular posts from this blog

RC CHALAMILA AWATAKA WENYEVITI NA WATENDAJI KATA NA MITAA DAR KUSIMAMIA ULINZI NA USALAMA.

MAHAFALI YA NANE SHULE YA AWALI NA MSINGI SAI YAFANA, WAZAZI WATAKIWA KULEA WATOTO KATIKA MISINGI YA MAADILI MEMA.