WAKILI DKT. MASOUD: TUADHIMISHE UHURU KWA KULINDA AMANI, KUONDOA UDINI NA KUJENGA UZALENDO.


Dar es Salaam,

Kuelekea maadhimisho ya  miaka 64 ya Uhuru wa Tanzania bara,Wakili Dkt. Khamis Masoud ametoa wito kwa Watanzania wote kuadhimisha siku hiyo kwa kuimarisha misingi ya amani, kuondokana na kauli za udini na kujenga moyo wa uzalendo unaoendeleza umoja wa kitaifa.


Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam, Dkt. Masoud amesema kauli zinazochochea misimamo ya kidini zina madhara makubwa kwa mustakabali wa taifa, kwani huibua mgawanyiko unaoweza kudhoofisha mshikamano ambao umeitambulisha Tanzania kwa miongo kadhaa.


“Maadhimisho ya Uhuru yanapaswa kutukumbusha thamani ya amani tuliyonayo. Ni wakati wa kuondoa kabisa kauli za udini na kujenga taifa lenye umoja, maridhiano na uelewano. Amani si jambo la kawaida; ni urithi tuliopewa na waasisi wetu na lazima tuihifadhi,” amesema.


Amesema ni wajibu wa viongozi wa dini kukemea maovu kama mafundisho ya vitabu vyao vinavyoelekeza, lakini kufanya hivyo kwa hekima na bila kuibua mgawanyiko wa kiimani. Aidha, amewataka waendelee kutimiza wajibu wao wa kuonya, kusihi na kuongoza jamii katika misingi ya upendo, amani na ustawi.


Katika kauli yake, Dkt. Masoud amesisitiza kuwa viongozi walioteuliwa na Rais, hususan wakuu wa mikoa na wilaya, wanapaswa kutambua uzito wa dhamana waliyokabidhiwa na kuhakikisha kauli zao zinajenga umoja na siyo kuzidisha migongano.


“Wakuu wa mikoa na wilaya ni wawakilishi wa Rais katika maeneo yao. Kauli zao zinapaswa kutuliza, kuunganisha na kupatanisha jamii. Mgawanyiko unaotokana na kauli za viongozi hauna manufaa kwa dola,” amebainisha.


Akizungumzia nafasi ya vyombo vya habari, Dkt. Masoud amesema waandishi wa habari ni mhimili muhimu katika ujenzi wa taifa, hivyo wanapaswa kutumia kalamu zao kuimarisha amani na kuonesha taswira chanya ya nchi ndani na nje ya mipaka.


“Vyombo vya habari vina wajibu wa kujenga taifa. Habari zinazochochea chuki au mgawanyiko zinaharibu umoja. Tuwe wazalendo, tuandike habari zenye maana kwa taifa,” amesisitiza.


Dkt. Masoud amesema maadhimisho ya Uhuru ni fursa ya taifa kutafakari tulikotoka, tulipo na tunakoelekea, huku akihimiza kujenga matumaini, kufanya kazi kwa bidii na kuimarisha mshikamano kwa vizazi vya sasa na vijavyo.


“Tunapoelekea kwenye maadhimisho ya Uhuru, tuhubiri amani, tuimarishe uzalendo na tuweke mbele maslahi ya taifa. Huu ni wakati wa kuziimarisha nguzo zinazolifanya taifa letu kuwa imara,” amesema.

Comments

Popular posts from this blog

RC CHALAMILA AWATAKA WENYEVITI NA WATENDAJI KATA NA MITAA DAR KUSIMAMIA ULINZI NA USALAMA.

MAHAFALI YA NANE SHULE YA AWALI NA MSINGI SAI YAFANA, WAZAZI WATAKIWA KULEA WATOTO KATIKA MISINGI YA MAADILI MEMA.