WAUMINI WA KANISA KATOLIKI WAIANDIKIA VATICAN WAKITAKA UCHUNGUZI WA MWENENDO WA PADRI KITIMA.


DAR ES SALAAM 

Waumini wawili wa Kanisa Katoliki nchini, Stanslaus Thobias Nyakunga na Elia Phaustine Kabote, wameiandikia Vatican kupitia Balozi wake nchini Tanzania, Archbishop Angelo Accattino, wakiomba kufanyika kwa uchunguzi wa kichungaji na kiutawala kuhusu mwenendo wa Padri Dkt. Charles Kitima, Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), wakieleza hofu ya Kanisa kuonekana kuhusishwa na misimamo ya vyama vya siasa.


Katika barua hiyo, waumini hao wameeleza kuwa kwa kipindi kirefu kumekuwapo mitazamo katika jamii inayodai kuwa Padri Kitima amekuwa akionekana kuingilia au kujihusisha na masuala ya siasa, hususan migogoro ya ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), jambo ambalo, kwa mujibu wao, halijajitokeza kwa kiwango kama hicho kwa vyama vingine vya siasa.


Wamefafanua kuwa madai hayo, bila kujali kama yana ukweli au la, yameanza kuathiri taswira ya Kanisa miongoni mwa waumini na kwa umma, hali inayoweza kulifanya Kanisa lionekane kama linachukua upande wa kisiasa, kinyume na jukumu lake la msingi la kuwa taasisi ya amani, maridhiano na mwongozo wa kimaadili.


Nyakunga na Kabote wamesisitiza kuwa hatua yao haikulenga kutoa tuhuma wala kumshambulia Padri Kitima binafsi, bali kuomba mamlaka ya juu ya Kanisa kuchunguza na kutoa mwongozo wa wazi, kwa hekima ya kichungaji, ili kulinda umoja wa waumini na heshima ya Kanisa.


Katika kuunga mkono hoja zao, waumini hao wamenukuu Maandiko Matakatifu yanayosisitiza wajibu wa viongozi wa Kanisa kuwa wajenzi wa amani na mshikamano, wakiwemo maneno ya Yesu Kristo yasemayo “Heri wapatanishi, maana hao wataitwa wana wa Mungu” (Mathayo 5:9), pamoja na kauli ya Mtume Paulo kwamba “Mungu si wa machafuko bali wa amani” (1 Wakorintho 14:33), na onyo dhidi ya migawanyiko miongoni mwa waumini (1 Wakorintho 1:10).


Hatua hiyo inachukuliwa katika kipindi ambacho nchi inapitia mjadala mpana wa kisiasa na kijamii, hali inayozidi kuongeza matarajio kwa taasisi za dini kubaki nguzo za utulivu, upatanisho na mshikamano wa kitaifa, bila kuingia katika mvutano wa vyama.


Kwa mujibu wa barua hiyo, waumini hao wameiomba Holy See kushughulikia masuala matatu makuu: kufanya uchunguzi wa kina kuhusu mwenendo wa Padri Kitima, kutoa mwelekeo wa wazi unaothibitisha uhuru wa uongozi wa Kanisa dhidi ya siasa za vyama, pamoja na kuchukua hatua zozote zitakazolinda umoja wa waumini, amani ya jamii na mamlaka ya kimaadili ya Kanisa.


Waumini hao wameeleza imani yao kwamba Vatican ina busara, uzoefu na mamlaka ya kushughulikia suala hilo kwa maslahi mapana ya Kanisa na jamii kwa ujumla.




Comments

Popular posts from this blog

RC CHALAMILA AWATAKA WENYEVITI NA WATENDAJI KATA NA MITAA DAR KUSIMAMIA ULINZI NA USALAMA.

MAHAFALI YA NANE SHULE YA AWALI NA MSINGI SAI YAFANA, WAZAZI WATAKIWA KULEA WATOTO KATIKA MISINGI YA MAADILI MEMA.