Waziri Mchengerwa Aagiza Kuanzishwa kwa “One Stop Digital Centre” Kurahisisha Huduma za Afya.


Na Mwandishi Wetu – Dar es Salaam


Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, ameagiza kutungwa na kuanza kutekelezwa kwa mfumo mpya wa kidijitali utakaoboreshwa kwa lengo la kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za afya nchini, hususan kupunguza foleni na kurahisisha upatikanaji wa huduma katika hospitali na vituo vya afya.


Akizungumza leo Desemba 8, 2025 katika kikao kazi na watumishi wa Sekta ya Afya kilichofanyika katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, jijini Dar es Salaam, Waziri Mchengerwa alisema ni wakati muafaka kwa Tanzania kuanzisha “One Stop Digital Centre” mfumo wa teknolojia ya afya utakaoimarisha hatua zote za huduma kuanzia usajili, malipo, hadi upatikanaji wa huduma.


Waziri alisema mfumo huo utaondoa adha ya wagonjwa kutumia muda mrefu wakizunguka katika maeneo mbalimbali ya hospitali, hatua ambayo imekuwa ikisababisha usumbufu kwa wananchi na kupunguza ufanisi wa watumishi wa afya.


Alifafanua kuwa mpangilio huo wa kidijitali utawezesha mgonjwa kupata huduma kwenye eneo moja, na hivyo kurahisisha mchakato mzima wa matibabu.


Aidha, alisisitiza kuwa mfumo huo utaboresha usimamizi na uhifadhi wa taarifa za wagonjwa, kuhakikisha kuwa kumbukumbu zinapatikana wakati wowote inapohitajika, jambo litakalosaidia kuongeza ubora wa huduma na kupunguza malalamiko ya upotevu au ucheleweshaji wa taarifa za kitabibu.


Katika agizo lake, Mhe. Mchengerwa ametoa muda wa siku 30 kwa wataalamu wa TEHAMA wa Wizara ya Afya kuandaa muundo wa mfumo huo na kuhakikisha kuwa utaweza kusomana na mifumo mingine katika ngazi zote za huduma kutoka zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya, hadi hospitali za mikoa.


Waziri alihitimisha kwa kusisitiza kuwa maboresho ya kidijitali ni msingi muhimu katika mageuzi ya sekta ya afya, na kwamba serikali imejipanga kuhakikisha huduma zinazotolewa zinakuwa za kisasa, zenye ufanisi na zinazomweka mgonjwa mbele kama kipaumbele cha msingi.


Comments

Popular posts from this blog

RC CHALAMILA AWATAKA WENYEVITI NA WATENDAJI KATA NA MITAA DAR KUSIMAMIA ULINZI NA USALAMA.

MAHAFALI YA NANE SHULE YA AWALI NA MSINGI SAI YAFANA, WAZAZI WATAKIWA KULEA WATOTO KATIKA MISINGI YA MAADILI MEMA.