DC KIBAHA AUPA MSUKUMO UVUNAJI ENDELEVU MISITUNI.


Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Mhe. Nickson Simon, amezitaka serikali za vijiji wilayani humo kuwa mstari wa mbele katika kulinda rasilimali za misitu kwa kuhakikisha mpango wa uvunaji endelevu wa mazao ya misitu unatekelezwa kikamilifu kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizopo.


Mhe. Simon alitoa msisitizo huo leo Januari 19, 2026, wakati wa Kikao cha Tathmini ya Nusu Mwaka (Julai–Desemba 2025) kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikoko, ofisi za Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Kanda ya Mashariki, wilayani Kibaha, mkoani Pwani.


Alisema vijiji vina jukumu la kutoa taarifa mara moja pale uvunaji unapobainika kufanyika kinyume cha taratibu, pamoja na kuwasilisha taarifa za wavunaji wanaokiuka sheria mara kwa mara, ili mamlaka zichukue hatua stahiki kwa mujibu wa sheria.


Katika kuimarisha usimamizi wa misitu, Mhe. Simon aliagiza asilimia 20 ya mapato yote yanayokusanywa ngazi ya kijiji itengwe kwa ajili ya kusimamia upandaji wa miti inayotolewa na TFS, akisisitiza umuhimu wa kuitunza ili ikue na kufikia malengo ya uhifadhi. Aidha, alielekeza vijiji kutenga asilimia tano (5) ya mapato hayo kwa ajili ya doria za kijiji, kama njia ya kuhakikisha sheria na taratibu za uvunaji zinasimamiwa ipasavyo.


Akizungumza kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi Tanzania, Profesa Dos Santos Silayo, Mhifadhi Necta Fatael Urio wa TFS alisema kikao hicho kimeandaliwa kwa lengo la kutathmini mwenendo wa uvunaji wa mazao ya misitu katika Wilaya ya Kibaha.


Urio alieleza kuwa tathmini hiyo inahusisha kiwango cha uvunaji kilichoruhusiwa katika nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha 2025/2026 (Julai–Desemba), ili kujiridhisha kama mpango wa uvunaji endelevu unatekelezwa kama ulivyopangwa.


Aliongeza kuwa kikao hicho pia kililenga kuhakiki utekelezaji wa vibali vya uvunaji, kuhakikisha wavunaji wote waliopata vibali walizingatia masharti, pamoja na kufanya marekebisho ya mpango wa uvunaji pale inapobidi, hususan kwa wavunaji waliokamilisha migao yao mapema, bila kuhatarisha uendelevu wa rasilimali za misitu.


Comments

Popular posts from this blog

RC CHALAMILA AWATAKA WENYEVITI NA WATENDAJI KATA NA MITAA DAR KUSIMAMIA ULINZI NA USALAMA.

MAHAFALI YA NANE SHULE YA AWALI NA MSINGI SAI YAFANA, WAZAZI WATAKIWA KULEA WATOTO KATIKA MISINGI YA MAADILI MEMA.