SHINYANGA YAJITOSHELEZA KWA CHAKULA – RC MHITA.


Shinyanga


Mkoa wa Shinyanga umeendelea kuimarisha usalama wa chakula baada ya kuzalisha tani 947,487 za mazao ya chakula katika msimu wa kilimo wa mwaka 2024/2025, kiasi kinachomuwezesha mkoa kuwa na ziada ya chakula tani 95,003.


Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, alipomkaribisha Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. David Silinde, aliyefika mkoani humo kwa ziara ya kikazi ya siku moja, ikiwa ni sehemu ya mazungumzo rasmi katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa.


Mhe. Mhita amesema mahitaji ya chakula kwa mkoa kwa mwaka ni tani 531,747, hivyo uzalishaji uliopo unathibitisha Shinyanga kujitosheleza kikamilifu kwa chakula, kulingana na idadi ya watu kufuatia Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022.


Ameongeza kuwa mafanikio hayo yametokana na juhudi za Serikali katika kuboresha sekta ya kilimo, ambapo pamoja na mazao ya chakula, uzalishaji wa zao la pamba umeongezeka kutoka tani 21,599 (msimu wa 2021/2022) hadi kufikia tani 34,689.22 (msimu wa 2024/2025).


Kutokana na mafanikio hayo, Mkuu wa Mkoa amemhakikishia Naibu Waziri kuwa mkoa utaendelea kuimarisha matumizi ya maafisa ugani 275 waliopo, ili kuhakikisha wakulima wanapatiwa elimu ya kilimo cha kisasa na chenye tija. Hatua hii itasaidia kuondokana na kilimo cha mazoea na kuongeza uzalishaji wa mazao.


Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Kilimo, Mhe. David Silinde, amempongeza Mkuu wa Mkoa kwa mapokezi mazuri pamoja na juhudi kubwa zinazofanywa na uongozi wa mkoa katika kuimarisha sekta ya kilimo.


Ziara yake ya siku moja mkoani Shinyanga ililenga kukagua bwawa la umwagiliaji la Nyida pamoja na kufanya ukaguzi wa zao la pamba, ili kujionea utekelezaji wa miradi ya kilimo mkoani humo.



Comments

Popular posts from this blog

RC CHALAMILA AWATAKA WENYEVITI NA WATENDAJI KATA NA MITAA DAR KUSIMAMIA ULINZI NA USALAMA.

MAHAFALI YA NANE SHULE YA AWALI NA MSINGI SAI YAFANA, WAZAZI WATAKIWA KULEA WATOTO KATIKA MISINGI YA MAADILI MEMA.