TMA YABAINISHA NJIA RASMI ZA UPATIKANAJI WA TAARIFA ZA HALI YA HEWA.
Zanzibar
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imebainisha na kufafanua njia rasmi zinazotumiwa kusambaza taarifa sahihi za hali ya hewa nchini, huku ikiwataka wananchi kuepuka kutegemea taarifa zisizo rasmi zinazochangia upotoshaji katika jamii.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa TMA – Ofisi ya Zanzibar, Ndg. Masoud Makame Faki, alipokuwa akizungumza na wananchi kupitia vyombo mbalimbali vya habari wakati akiwakaribisha kutembelea banda la TMA lililopo katika Maonesho ya 12 ya Kimataifa ya Biashara Zanzibar (ZITF), yanayoendelea kufanyika katika Viwanja vya Nyamanzi kuanzia tarehe 29 Desemba 2025 hadi 16 Januari 2026.
Akizungumza katika maonesho hayo, Ndg. Faki alisema TMA imekuwa ikitoa taarifa sahihi na za uhakika za hali ya hewa kupitia njia rasmi zilizorasimishwa, ikiwemo vyombo vya habari, blogu, tovuti ya Mamlaka (www.meteo.go.tz) pamoja na kurasa za mitandao ya kijamii za TMA zikiwemo YouTube, Instagram, Twitter (X), WhatsApp Channel na Facebook, ambazo zote zimeunganishwa moja kwa moja kupitia ukurasa wa mwanzo wa tovuti ya Mamlaka.
“Ninawasisitiza wananchi kuendelea kufuatilia taarifa za hali ya hewa kupitia vyanzo rasmi vya Mamlaka ili kupata taarifa sahihi na za uhakika. Taarifa zisizo rasmi zinazosambazwa mitandaoni zinaweza kuleta taharuki na athari katika mipango ya maendeleo ya nchi,” alisema.
Aidha, Ndg. Faki alitoa wito kwa wananchi kuachana na tabia ya kusambaza na kuamini taarifa potofu za hali ya hewa, akibainisha kuwa hatua hiyo inaweza kusababisha maamuzi yasiyo sahihi katika shughuli za kijamii na kiuchumi.
Kupitia banda lao la maonesho katika ZITF, TMA imeendelea kutoa elimu ya kina kuhusu masuala ya hali ya hewa, ikiwemo kutoa ufafanuzi juu ya ongezeko la joto linaloendelea kushuhudiwa visiwani Zanzibar. Alifafanua kuwa kwa sasa dunia inapokuwa katika mzunguko wake kuelekea kwenye kizio cha kusini, kunakuwa na jua la utosi linalochochea ongezeko la joto. Aidha, kutokana na Zanzibar kuzungukwa na maji, kiwango cha unyevu hewani huongezeka na kusababisha wakazi kuhisi fukuto kubwa la joto.
Mwisho, alihimiza wananchi kuendelea kujitokeza katika banda la TMA kupata elimu zaidi kuhusu huduma mbalimbali za hali ya hewa, matumizi yake katika sekta za kijamii na kiuchumi, pamoja na namna bora ya kuzitumia taarifa hizo kwa manufaa ya maendeleo ya Taifa.



Comments
Post a Comment