TNCC YANG’ARA ZITF: RC KUSINI UNGUJA AFURAHISHWA NA HUDUMA BORA ZA BIASHARA.

Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Mhe. Hamida Mussa Khamis Shuduma, ameipongeza Chemba ya Taifa ya Biashara Tanzania (TNCC) kwa huduma zake zenye mchango mkubwa katika kukuza biashara na uchumi, hususan huduma ya Certificate of Origin.
Akizungumza baada ya kutembelea banda la TNCC katika Maonesho ya Kimataifa ya Biashara Zanzibar (Zanzibar International Trade Fair – ZITF), Mhe. Hamida alisema huduma ya Certificate of Origin ni nyenzo muhimu inayowezesha wafanyabiashara kufanya shughuli za kimataifa kwa urahisi na kuaminika.
Aidha, Mkuu wa Mkoa alipendekeza wananchi wa Kusini Unguja kuhamasishwa kupitia mabaraza ya biashara ili kuielewa na kuitumia huduma hiyo ipasavyo, akibainisha kuwa hatua hiyo itawawezesha kunufaika zaidi na fursa za masoko ya ndani na nje ya nchi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa TNCC, Bw. Matina Nkurlu, alisema taasisi hiyo itaendelea kutoa huduma zenye tija kwa wafanyabiashara ili kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya kimataifa.
“TNCC inaendelea kujikita katika kuwahudumia wafanyabiashara kwa kutoa huduma zenye tija, ikiwemo Certificate of Origin, ambayo ni chachu ya kufungua masoko ya kimataifa na kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania,” alisema Bw. Nkurlu.


Comments
Post a Comment