UJENZI WA BOMBA LA MAFUTA GHAFI LA AFRIKA MASHARIKI WAFIKIA ASILIMIA 79.


Dar es Salaam.

Ujenzi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) umefikia asilimia 79, huku mradi huo wa kimkakati ukitarajiwa kukamilika mwezi Julai 2026 na kuchochea ukuaji wa uchumi pamoja na kutoa maelfu ya ajira kwa wananchi wa Tanzania na Uganda.


Hatua hiyo imeelezwa wakati wa ziara rasmi ya Waziri wa Nishati na Maendeleo ya Madini wa Uganda, Dkt. Ruth Nankabirwa, aliyeko nchini kukagua maendeleo ya mradi huo unaosafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani mkoani Tanga, kwa kushirikiana na mwenyeji wake, Waziri wa Nishati wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi.


Akizungumza na waandishi wa habari, Mhe. Ndejembi amesema utekelezaji wa mradi wa EACOP umechangia kwa kiasi kikubwa katika utoaji wa ajira, ambapo ajira zaidi ya 12,000 zimetolewa kwa vijana na wananchi wa nchi hizo mbili tangu kuanza kwa ujenzi.


Amesema mradi huo utakapokamilika utakuwa na uwezo wa kusafirisha mapipa 246,000 ya mafuta ghafi kwa siku, hali itakayoongeza mapato ya serikali, kuimarisha uchumi wa kikanda na kuongeza mchango wa sekta ya nishati katika maendeleo ya Taifa.


Kwa upande wake, Dkt. Nankabirwa amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa uongozi wake thabiti na dhamira ya dhati katika kuhakikisha mradi huo wa kimkakati unatekelezwa kwa mafanikio.


Amesema mradi wa EACOP umeleta mabadiliko makubwa ya kiuchumi katika ukanda wa Afrika Mashariki na kusisitiza umuhimu wa kuwepo kwa mfumo maalumu wa kuwatambua wafanyakazi waliopata uzoefu katika miradi mikubwa ya kimkakati, ili waweze kupewa kipaumbele katika utekelezaji wa miradi mingine ijayo ikiwemo ya gesi asilia na umeme.




Comments

Popular posts from this blog

RC CHALAMILA AWATAKA WENYEVITI NA WATENDAJI KATA NA MITAA DAR KUSIMAMIA ULINZI NA USALAMA.

MAHAFALI YA NANE SHULE YA AWALI NA MSINGI SAI YAFANA, WAZAZI WATAKIWA KULEA WATOTO KATIKA MISINGI YA MAADILI MEMA.