WAZIRI WA MASUALA YA JAMII DRC ATEMBELEA KAMBI YA WAKIMBIZI NYARUGUSU.


Ujumbe kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ukiongozwa na Waziri wa Nchi anayeshughulikia masuala ya Ustawi wa Jamii, Hatua za Kibinadamu na Mshikamano, Mhe. Eve Bazaiba Masudi, umetembelea Kambi ya Wakimbizi ya Nyarugusu, mkoani Kigoma, kwa lengo la kujionea hali ya maisha ya wakimbizi na kusikiliza maoni pamoja na mapendekezo yao kwa Serikali ya DRC.


Katika ziara hiyo, Mhe. Masudi aliishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuendelea kutoa hifadhi kwa wakimbizi kutoka DRC kwa takribani miaka 30 sasa, tangu kambi hiyo ilipoanzishwa. Amesema Tanzania imekuwa kisiwa cha amani na utu, na kwamba ukarimu huo umechangia kulinda hadhi ya watu waliolazimika kukimbia kutokana na changamoto mbalimbali nchini mwao.


Aidha, Waziri huyo ameeleza kuwa Serikali ya DRC inaendelea na jitihada za kutafuta suluhisho la kudumu la kurejesha amani, ili wakimbizi waweze kurejea nchini mwao kwa hiari. Amehimizwa wakimbizi kuishi kwa nidhamu na kuzingatia maadili, ili kulinda heshima ya nchi yao na kuthamini ukarimu wa Serikali ya Tanzania.


Vilevile, Mhe. Masudi amewataka wakimbizi walio tayari kurejea nchini mwao kuendelea kujisajili rasmi ili kurahisisha mchakato wa kurejea nyumbani na kuanza shughuli za maendeleo katika maeneo yao.


Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. James Milya, amesema Serikali ya Tanzania itaendelea kusimamia misingi ya sheria za kimataifa za ulinzi wa wakimbizi na kushirikiana nao katika kipindi chote cha mpito cha kurejea kwao. Amesisitiza kuwa kurejea nyumbani ni hiari na siyo shuruti, huku akiwahakikishia usalama katika mchakato huo.


Akiwasilisha taarifa ya kambi, Kaimu Mkuu wa Kambi ya Nyarugusu, Bw. Samwel Kuyi, amesema kwa sasa kambi hiyo inahifadhi jumla ya wakimbizi 132,404, ambapo kati yao 86,918 wanatoka DRC, 45,346 ni Warundi, na 98 wanatoka mataifa mengine. Aidha, zaidi ya asilimia 60 ya wakimbizi wa DRC ni watoto chini ya miaka 18, huku 21,660 wakiwa ni watoto walio chini ya miaka mitano.


Mmoja wa wakimbizi, Apolina Masumbuko, ameeleza kuwa wako tayari kurejea nchini mwao endapo Serikali ya DRC itarejesha amani na usalama, ili warudi katika mazingira tulivu.




Comments

Popular posts from this blog

RC CHALAMILA AWATAKA WENYEVITI NA WATENDAJI KATA NA MITAA DAR KUSIMAMIA ULINZI NA USALAMA.

MAHAFALI YA NANE SHULE YA AWALI NA MSINGI SAI YAFANA, WAZAZI WATAKIWA KULEA WATOTO KATIKA MISINGI YA MAADILI MEMA.