WANAHABARI: SAUTI MUHIMU KWENYE SULUHISHO LA MABADILIKO YA TABIA NCHI.


Na Fidea Masunga.


Mabadiliko ya tabianchi yanagusa kila mtu, na vyombo vya habari vina jukumu la kipekee kuhakikisha hatua za kukabiliana na mabadiliko haya zinafanyika kwa haki, zinashirikisha wananchi, na kuwahimiza viongozi kuwajibika.


Hayo yamebainishwa kwenye kongamano la kimtandao la Cross Border Science CafĂ©, lililoandaliwa na Media for Environment, Science, Health and Agriculture (MESHA) kwa kushirikiana na International Development Research Centre (IDRC). Kongamano hilo liliwakutanisha wanahabari na wadau kutoka nchi sita za Afrika kujadili mabadiliko ya tabianchi, jinsia, afya, na habari zenye matokeo chanya kwa jamii.


Teresa Anderson, Kiongozi wa Kimataifa wa Haki ya Tabianchi wa ActionAid International, alisema nishati safi ni suluhisho la kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, lakini inahitaji mshikamano wa wadau wote, wakiwemo wanahabari, wakati wa utekelezaji wa sera za tabianchi. “Sera za tabianchi lazima ziwe sawa, zikihakikisha chakula, nishati na ardhi vinabaki salama kwa wote. Serikali zina jukumu la kuhakikisha kanuni hizi zinafuatwa,” alisema.


Imali Ngusale, Kiongozi wa Mkakati na Masuala ya Kiufundi wa Africa Centre for Health, Climate and Gender Advocacy (ACHCGA), alisema mabadiliko ya tabianchi yanaathiri kila mtu tofauti kulingana na jinsia na umri. “Sera za mabadiliko ya tabianchi lazima ziwe jumuishi na zenye uwajibikaji, ili hakuna anayebaki nyuma,” alisema.


Audrey Masitsa, Meneja wa Mawasiliano wa Mission Inclusion, alisema mabadiliko ya tabianchi hayana upendeleo wa kijinsia, lakini wanawake wamekuwa waathirika wakubwa. “Wanakabiliwa na changamoto za upatikanaji wa nishati ya kupikia, maji, na chakula. Ni jukumu la wanahabari kuhakikisha habari zinazochapishwa zinawakilisha sauti za wanawake, vijana, na makundi yaliyo pembezoni,” alisema.


Violet Otindo, mtaalamu wa mawasiliano ya sayansi na mazingira kutoka MESHA, alisema ni muhimu kuhakikisha mjadala wa tabianchi unawafikia wananchi kwa lugha rahisi, yenye mvuto, na inayovutia. Alisisitiza kuwa habari zinapaswa kuangazia sauti za wanawake, vijana, na makundi yaliyo pembezoni, ili sera za tabianchi ziwe jumuishi na zenye uwajibikaji.


Aliongeza kuwa vyombo vya habari vina nguvu ya kipekee kuibua fursa, kuhamasisha hatua za kijamii na kiuchumi, na kuonyesha kuwa suluhisho la mabadiliko ya tabianchi si dogo. “Hali hii inaweza kuleta manufaa makubwa kwa jamii na kuunda mustakabali endelevu kwa vizazi vijavyo,” alisema Violet.


Comments

Popular posts from this blog

RC CHALAMILA AWATAKA WENYEVITI NA WATENDAJI KATA NA MITAA DAR KUSIMAMIA ULINZI NA USALAMA.

MAHAFALI YA NANE SHULE YA AWALI NA MSINGI SAI YAFANA, WAZAZI WATAKIWA KULEA WATOTO KATIKA MISINGI YA MAADILI MEMA.