TMA YATABIRI BARIDI MSIMU WA KIPUPWE 2026, YATOA TAHADHARI YA MVUA ZA EL NINO
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema msimu wa kipupwe wa Juni hadi Agosti 2026 unatarajiwa kutawaliwa na hali ya baridi ya wastani hadi kali katika maeneo mbalimbali ya nchi, huku ikitoa tahadhari ya uwezekano wa mvua kubwa zinazoweza kusababishwa na hali ya El Niño kuelekea Oktoba hadi Desemba mwaka huu.
Akizungumza na Waandishi wa habari kuhusu mwelekeo wa msimu wa kipupwe (JJA) 2026, Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Ladislaus Chang’a alisema vipindi vya baridi kali zaidi vinatarajiwa mwezi Julai hususan katika Nyanda za Juu Kusini Magharibi, Ukanda wa Ziwa Victoria na maeneo ya Magharibi mwa nchi.
Aidha, alisema maeneo ya pwani ya kaskazini pamoja na Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki yanatarajiwa kuwa na hali ya joto kiasi hadi baridi ya wastani, huku baadhi ya maeneo yakipata mvua za nje ya msimu licha ya kuwepo katika kipindi cha ukavu.
Chang’a alieleza kuwa mvua hizo zinaweza kujitokeza zaidi Ukanda wa Ziwa Victoria, pwani ya Bahari ya Hindi na maeneo ya miinuko ya Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki.
Kutokana na hali hiyo, TMA imetoa wito kwa wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya athari za baridi, magonjwa yanayohusiana na hali ya hewa pamoja na uwezekano wa mvua kubwa, huku wadau wa sekta mbalimbali wakihimizwa kufuatilia kwa karibu taarifa za mara kwa mara za utabiri wa hali ya hewa.




Comments
Post a Comment