TAKUKURU KINONDONI YADHIBITI UPOTEVU WA ZAIDI YA SHILINGI MILIONI 563.
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kinondoni imefanikiwa kudhibiti upotevu wa mapato ya Serikali yenye thamani ya zaidi ya Shilingi milioni 563 kupitia ufuatiliaji wa ukusanyaji wa ushuru wa huduma (Service Levy).
Akizungumza na waandishi wa habari, Naibu Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Kinondoni, Elizabeth Mokiwa amesema mafanikio hayo yamepatikana katika kipindi cha Januari hadi Machi 2026 baada ya kubaini baadhi ya wafanyabiashara kutolipa ushuru wa huduma kwa mujibu wa Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa.
Amesema baada ya ufuatiliaji huo, wafanyabiashara husika walitakiwa kulipa madeni yao kupitia control namba za Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, ambapo jumla ya Shilingi 563,663,820.15 zililipwa kutoka kampuni mbalimbali.
Katika kipindi hicho, TAKUKURU pia ilifuatilia miradi saba ya maendeleo katika sekta za afya na elimu ili kuhakikisha inatekelezwa kwa ubora na kwa kuzingatia matumizi sahihi ya fedha za Serikali.
Aidha, wananchi 6,571 walifikishwa elimu ya kupinga rushwa kupitia semina, mikutano ya hadhara, vipindi vya redio na televisheni pamoja na klabu za wapinga rushwa mashuleni na vyuoni.
TAKUKURU imesema itaendelea kuimarisha mapambano dhidi ya rushwa na kuwataka wananchi kutoa taarifa za vitendo vya rushwa kupitia ofisi zake au simu ya bure 113.


Comments
Post a Comment