TMA, EMEDO WAZINDUA TUZO ZA WANAHABARI KUHAMASISHA ELIMU YA HALI YA HEWA.


Na Mwandishi Wetu

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kwa kushirikiana na Shirika la Usimamizi wa Mazingira na Maendeleo (EMEDO) wamezindua rasmi Tuzo za Waandishi wa Habari zinazolenga kuhamasisha elimu ya hali ya hewa, tahadhari za mapema pamoja na usalama majini nchini.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Mbezi Garden jijini Dar es Salaam, Afisa Uchechemuzi wa EMEDO, Mary Francis Mahemba alisema vyombo vya habari vina mchango mkubwa katika kuelimisha jamii kuhusu changamoto za hali mbaya ya hewa na hatua za kujikinga dhidi ya majanga.

Alisema kupitia tuzo hizo, taasisi hizo zinalenga kutambua mchango wa wanahabari katika kusambaza taarifa sahihi zinazosaidia kuokoa maisha ya wananchi na kuongeza uelewa kuhusu usalama majini.

“Waandishi wa habari ni wadau muhimu katika kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi na kwa wakati kuhusu tahadhari za hali ya hewa, usalama majini na hatua za kujikinga dhidi ya majanga,” alisema Mahemba.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, tuzo hizo zitahusisha kazi za habari zinazohusu matukio ya hali mbaya ya hewa na athari zake kwa jamii, tahadhari za mapema za hali ya hewa, usalama wa usafiri majini, uzuiaji wa ajali za kuzama maji pamoja na ustahimilivu wa jamii dhidi ya majanga yanayotokana na mabadiliko ya tabianchi.

TMA na EMEDO zimesema tuzo hizo zitawahusisha waandishi kutoka redio, televisheni, magazeti, mitandao ya kijamii pamoja na majukwaa mbalimbali ya kidijitali nchini.

Waandishi wa habari wametakiwa kuwasilisha kazi zao zilizochapishwa au kurushwa hewani ndani ya kipindi cha kuanzia Agosti 1, 2025 hadi Agosti 30, 2026 kupitia barua pepe za media@meteo.go.tz na mediahaliyahewa@gmail.com.

Kwa upande wake, Meneja Masoko na Uhusiano wa TMA, Monica Mutoni alisema mamlaka hiyo itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuongeza thamani ya tuzo hizo na kuhamasisha matumizi ya taarifa za hali ya hewa katika shughuli za kijamii na kiuchumi.

Alisema taarifa za tahadhari za mapema zimeendelea kuwa nyenzo muhimu katika kuokoa maisha ya wananchi, hususan kwa jamii zinazotegemea shughuli za uvuvi na usafiri wa majini.

Ushirikiano huo kati ya TMA na EMEDO umetajwa kuwa sehemu ya juhudi za kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi za umma, mashirika ya kiraia na vyombo vya habari katika kukuza uelewa na matumizi sahihi ya taarifa za hali ya hewa nchini.




Comments

Popular posts from this blog

RC CHALAMILA AWATAKA WENYEVITI NA WATENDAJI KATA NA MITAA DAR KUSIMAMIA ULINZI NA USALAMA.

MAHAFALI YA NANE SHULE YA AWALI NA MSINGI SAI YAFANA, WAZAZI WATAKIWA KULEA WATOTO KATIKA MISINGI YA MAADILI MEMA.