WCF YAWAJENGEA UWEZO WANAHABARI KUHUSU MFUMO WA FIDIA NA HAKI ZA WAFANYAKAZI.
MFUKO wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) umeendelea kuimarisha utoaji wa elimu kuhusu haki za fidia kwa wafanyakazi kwa kuwapatia mafunzo waandishi wa habari, hatua inayolenga kuongeza uelewa wa masuala ya ulinzi wa kijamii na hifadhi ya jamii nchini.
Mafunzo hayo maalum yamefanyika jijini Dar es Salaam kwa ushirikiano wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) pamoja na Chama cha Waandishi wa Habari wanaofanya kazi katika Vyombo vya Habari Tanzania (JOWUTA).
Akizungumza katika ufunguzi wa mafunzo hayo, Rais wa TUCTA, Tumaini Nyamhokya alisema elimu hiyo ni muhimu katika kuwawezesha wanahabari kuelewa kwa kina masuala ya fidia kwa wafanyakazi ili waweze kuhabarisha jamii kwa usahihi zaidi.
Alisema WCF ni taasisi muhimu inayolinda wafanyakazi wanaopata madhila kazini ikiwemo ajali, magonjwa au vifo vinavyotokana na kazi zao, hivyo ipo haja ya jamii kupewa elimu ya kutosha kuhusu huduma zinazotolewa na mfuko huo.
Nyamhokya aliwataka waandishi wa habari kutumia taaluma yao kuelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kujiunga na mifuko ya hifadhi ya jamii pamoja na kuhakikisha waajiri wanatekeleza wajibu wao wa kuwasilisha michango na taarifa za matukio ya kazini kwa wakati.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa JOWUTA, Musa Juma Siwayombe alisema mafunzo hayo yamekuja wakati muafaka kutokana na changamoto zinazowakabili wanahabari wengi nchini, hususan ukosefu wa ajira za kudumu na mikataba isiyo rasmi katika baadhi ya vyombo vya habari.
Alisema hali hiyo imekuwa ikiwanyima wanahabari wengi fursa ya kupata ulinzi wa hifadhi ya jamii pamoja na haki nyingine muhimu za wafanyakazi.
“Wanahabari wanapaswa kuelewa haki zao za msingi ili waweze kujilinda na pia kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa mifumo ya fidia kwa wafanyakazi,” alisema Siwayombe.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Mahusiano kwa Umma wa WCF, Raula Kunenge alisema taasisi hiyo itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha wafanyakazi wanapata elimu sahihi kuhusu haki zao za fidia pamoja na huduma zinazotolewa na mfuko huo.
Kunenge alisema wanahabari wana nafasi kubwa ya kuifikisha elimu hiyo kwa jamii kupitia vyombo vya habari, hivyo ni muhimu kuwa na uelewa wa kutosha kuhusu sheria, taratibu na mafao yanayotolewa na WCF.
“Tunatarajia waandishi wa habari watakuwa mabalozi wazuri wa kuelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa ulinzi wa wafanyakazi na hatua za kuchukua pale ajali au madhara yanapotokea sehemu za kazi,” alisema Kunenge.
Mafunzo hayo pia yamelenga kuwapa washiriki uelewa kuhusu mafao mbalimbali yanayotolewa na WCF ikiwemo matibabu, fidia ya ulemavu, malipo ya wategemezi, msaada wa mazishi pamoja na huduma za utengemao.
Aidha, washiriki wamehimizwa kuwa mabalozi wa elimu ya fidia kwa wafanyakazi katika vyombo vyao vya habari ili kuongeza uelewa kwa jamii kuhusu haki za wafanyakazi na umuhimu wa ulinzi wa kijamii nchini.





Comments
Post a Comment