BARAZA JIPYA LA NIT LATAKIWA KUIMARISHA TAFITI NA MAFUNZO YA UCHUKUZI


Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, ameliagiza Baraza la 13 la Uongozi la National Institute of Transport kuhakikisha linasimamia kwa ufanisi mafunzo na tafiti zinazolenga kutatua changamoto za sekta ya usafirishaji na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.


Akizindua baraza hilo mkoani Morogoro, Prof. Mbarawa amesema chuo kina wajibu mkubwa wa kuisaidia Serikali katika kuandaa sera na mikakati madhubuti ya maendeleo ya sekta ya uchukuzi nchini.


Amesema utekelezaji wa jukumu hilo utawezesha chuo kufikia malengo ya mpango wake wa miaka mitano unaolenga kuboresha ubora wa elimu na mafunzo, kukidhi mahitaji ya soko la ajira la kisasa pamoja na kuimarisha miundombinu ya kujifunzia ikiwemo maabara, maktaba na matumizi ya teknolojia za kisasa.


Prof. Mbarawa ameongeza kuwa maandalizi ya awali ya Sera Mpya ya Taifa ya Uchukuzi yameanza kuzingatia mifumo mipya ya usafiri kama Cable Transport na Space Transport, hivyo akalitaka baraza hilo kuandaa wataalamu watakaoweza kuhudumia maeneo hayo yanayoibukia duniani.


Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa NIT, Dkt. Prosper Mgaya, amesema katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita chuo kimeanzisha kozi nane za kimkakati katika ngazi za uzamili, shahada na stashahada.


Amesema pia chuo kimeanzisha Kituo cha Umahiri cha Mafunzo ya Taaluma za Usafiri wa Anga na Operesheni za Usafirishaji (COEATO), kimenunua ndege mbili za mafunzo na kuanza kutoa mafunzo ya urubani kwa wanafunzi 22.


Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la 13 la Uongozi la NIT, Prof. Ulingata Mbamba, amesema baraza hilo litaendelea kusimamia utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya chuo, kuimarisha utawala bora na kuhakikisha matumizi sahihi ya rasilimali ili kuendelea kuzalisha wataalamu wenye ujuzi unaohitajika katika soko la ajira la kisasa.



Comments

Popular posts from this blog

RC CHALAMILA AWATAKA WENYEVITI NA WATENDAJI KATA NA MITAA DAR KUSIMAMIA ULINZI NA USALAMA.

MAHAFALI YA NANE SHULE YA AWALI NA MSINGI SAI YAFANA, WAZAZI WATAKIWA KULEA WATOTO KATIKA MISINGI YA MAADILI MEMA.