DKT. ABBASI AFUNGUA KIKAO CHA PILI CHA BODI YA USIMAMIZI WA MRADI WA MAENDELEO YA MISITU NA MNYORORO WA THAMANI.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi akiwa na Mwenyekiti mwenza ambaye ni Naibu Balozi wa Finland Bw. Tomi Lounio, wameongoza Kikao cha Pili cha Bodi ya Usimamizi wa Mradi wa Maendeleo ya Matumizi ya Ardhi, Misitu na Mnyororo wa Thamani(FORLAND).
Akizungumza katika kikao hicho, Dkt. Abbasi amesema ushirikiano unaoendelea kati ya Serikali za Tanzania na Finland unaonesha dhamira ya pamoja ya kukuza maendeleo endelevu, hususan kwa wakulima wadogo wa miti na jamii zinazoshiriki katika usimamizi wa misitu.
Aidha, ameeleza kuwa moja ya ajenda muhimu za kikao hicho ni kupitia na kujadili Rasimu ya Mpango Kazi na Bajeti ya mwaka 2026/2027, ambayo itaelekeza vipaumbele, shughuli na matumizi ya rasilimali kwa mwaka ujao.
Dkt. Abbasi amewahimiza wajumbe kutoa mchango wao wa kitaalamu ili kuhakikisha mradi unaendelea kuwa jumuishi, rafiki kwa mazingira na wenye manufaa ya kiuchumi kwa jamii, huku ukichochea uhifadhi na usimamizi bora wa rasilimali za misitu nchini.
“Kwa pamoja tunaweza kujenga uchumi imara unaotegemea misitu kwa manufaa ya watu na mazingira,” amesema Dkt. Abbasi.
Kikao hicho kimefanyika leo Juni 22, 2026 katika Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT) Dar es salaam.



Comments
Post a Comment