Dkt. Seif: Mazao ya Nyuki Ni Hazina ya Afya, Uchumi na Uhifadhi wa Mazingira.



Na Mwandishi Wetu, Dodoma


NAIBU Waziri wa Ofisi ya Rais – TAMISEMI anayeshughulikia masuala ya Afya, Dkt. Jafari Rajabu Seif, amepongeza juhudi za Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) katika kuendeleza sekta ya ufugaji nyuki na uzalishaji wa mazao yake, akisema sekta hiyo ina mchango mkubwa katika kuboresha afya za wananchi, kukuza uchumi na kuhifadhi mazingira.


Dkt. Seif alitoa pongezi hizo leo June 03,2026 baada ya kutembelea banda la TFS katika Maonesho ya Wiki ya Mazingira yanayoendelea katika Viwanja vya Ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma, ambako alipata fursa ya kujionea shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na wakala huo, hususan katika ufugaji nyuki na uchakataji wa mazao yatokanayo na nyuki.


Akiwa katika banda hilo, Naibu Waziri huyo alivutiwa na bidhaa mbalimbali zilizokuwa zikionyeshwa, zikiwemo asali, nta na bidhaa nyingine za nyuki ambazo zimeendelea kupata soko kutokana na ubora wake pamoja na manufaa yake katika afya, lishe na uchumi wa wananchi.


“Nimevutiwa sana na mazao ya nyuki niliyoyaona hapa. Bidhaa hizi zina manufaa makubwa kiafya na kiuchumi. Nawapongeza TFS kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuhamasisha wananchi kutumia rasilimali hizi kwa njia endelevu. Mimi mwenyewe nitakuwa mdau wa mazao haya kutokana na ubora wake na faida zake,” alisema Dkt. Seif.


Alisema sekta ya ufugaji nyuki ni miongoni mwa shughuli zinazoweza kuchangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa uchumi wa taifa sambamba na kuinua kipato cha wananchi, hususan jamii zinazoishi jirani na maeneo ya misitu.


Aidha, aliwataka wananchi kushiriki kikamilifu katika juhudi za uhifadhi wa mazingira na matumizi endelevu ya rasilimali za asili ili kuhakikisha misitu na bioanuwai vinaendelea kuwepo kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.


Kwa upande wake, TFS imeendelea kutumia maonesho hayo kutoa elimu kwa umma kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa misitu, ufugaji nyuki na matumizi ya bidhaa zitokanazo na nyuki kama sehemu ya kukuza uchumi wa kijani na kuimarisha ustawi wa wananchi.


Maonesho ya Wiki ya Mazingira mwaka huu yalianza Juni 1 na yanatarajiwa kuhitimishwa Juni 5, 2026, yakiwakutanisha wadau mbalimbali wa mazingira, taasisi za serikali, sekta binafsi na wananchi kwa lengo la kuhamasisha uhifadhi wa mazingira na matumizi endelevu ya rasilimali za asili.



Comments

Popular posts from this blog

RC CHALAMILA AWATAKA WENYEVITI NA WATENDAJI KATA NA MITAA DAR KUSIMAMIA ULINZI NA USALAMA.

MAHAFALI YA NANE SHULE YA AWALI NA MSINGI SAI YAFANA, WAZAZI WATAKIWA KULEA WATOTO KATIKA MISINGI YA MAADILI MEMA.