MAMIA YA WATANZANIA TABORA KUNUFAIKA NA UPASUAJI WA MTOTO WA JICHO BILA MALIPO
Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya afya, ikiwemo Helen Keller International, imeanzisha kambi maalum ya uchunguzi na upasuaji wa mtoto wa jicho katika Hospitali ya Wilaya ya Igunga mkoani Tabora, ambapo takribani wananchi 700 wanatarajiwa kunufaika na huduma hizo bila malipo.
Miongoni mwa wanufaika ni Henry Machibya (62), mkazi wa Simbo wilayani Igunga, ambaye amesema tatizo la macho lilianza mwaka 2023 na kuendelea kuathiri uwezo wake wa kuona hadi kupoteza kabisa uwezo wa kuona kwa macho yote mawili katika miezi ya hivi karibuni.
Machibya amesema hali hiyo ilimlazimu kuacha shughuli zake za kilimo ambazo zilikuwa chanzo chake kikuu cha mapato na kujikuta akitegemea msaada wa watu wa karibu katika kutekeleza mahitaji ya msingi ya kila siku.
“Nilikuwa nikitegemea kilimo kwa ajili ya kujikimu na kuhudumia familia yangu, lakini hali ya macho yangu ilibadilisha maisha yangu kabisa,” amesema.
Aidha, amesema changamoto nyingine alizokumbana nazo ni kushindwa kutambua chakula anachokula, kusindikizwa kwenda maeneo mbalimbali na kupoteza uhuru wa kufanya shughuli zake za kawaida.
Kupitia kambi hiyo ya uchunguzi na matibabu ya mtoto wa jicho inayofanyika katika Hospitali ya Wilaya ya Igunga, Machibya ameanza kupata huduma za kibingwa zinazolenga kurejesha uwezo wake wa kuona na kuendelea na shughuli za uzalishaji.
Wananchi wenye changamoto za macho wamehimizwa kujitokeza mapema kupata uchunguzi na matibabu bila malipo kupitia kambi hiyo iliyowezeshwa na ushirikiano kati ya Ofisi ya Rais TAMISEMI, Wizara ya Afya na Helen Keller International kwa lengo la kurejesha nuru na matumaini kwa mamia ya wakazi wa mkoa wa Tabora.



Comments
Post a Comment