SERIKALI YAAHIDI KUIMARISHA MAPAMBANO DHIDI YA BIDHAA BANDIA KULINDA AFYA NA UCHUMI WA TAIFA.
Serikali imeahidi kuendelea kuimarisha mapambano dhidi ya bidhaa bandia nchini ili kulinda afya za wananchi, kukuza biashara halali na kuimarisha uchumi wa taifa.
Ahadi hiyo imetolewa katika kilele cha Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Kudhibiti Bidhaa Bandia Duniani yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, ambapo Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda, alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kama mgeni rasmi wa maadhimisho hayo.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mapunda alisema bidhaa bandia zimeendelea kuwa tishio kubwa kwa afya za wananchi, ustawi wa biashara halali na uchumi wa taifa. Amesema bidhaa hizo husababisha madhara kwa watumiaji pamoja na kupunguza mapato ya serikali kutokana na biashara zisizo rasmi.
Mapunda alisisitiza kuwa mapambano dhidi ya bidhaa bandia hayawezi kuachiwa taasisi moja pekee, bali yanahitaji ushirikiano wa pamoja kati ya serikali, sekta binafsi, wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla. Aliongeza kuwa Serikali imeielekeza Tume ya Ushindani (FCC) kuendelea kutumia teknolojia za kisasa katika uchunguzi, ufuatiliaji na udhibiti wa bidhaa bandia, hususan katika masoko ya kidijitali na mipaka ya nchi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Ushindani, Jaji Rose Ibrahim, alisema bidhaa bandia zinaendelea kuhatarisha maisha ya wananchi na kuathiri mazingira ya biashara halali nchini. Alitoa wito kwa wananchi kuwa makini wanaponunua bidhaa mbalimbali na kutoa taarifa kwa mamlaka husika wanapobaini bidhaa zinazotiliwa shaka.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa FCC, Khadija Ngasongwa, alisema maadhimisho ya mwaka huu yamelenga kuongeza uelewa wa umma kuhusu madhara ya pombe, sigara na vilainishi bandia. Alisisitiza kuwa mapambano dhidi ya bidhaa bandia ni jukumu la kila mmoja katika jamii.
Kuelekea maadhimisho hayo, FCC ilifanya shughuli mbalimbali za kutoa elimu kwa umma kuhusu madhara ya bidhaa bandia na umuhimu wa kununua bidhaa halali.
Miongoni mwa shughuli hizo ni mikutano ya hadhara, kampeni za uhamasishaji katika masoko makubwa pamoja na utoaji wa elimu kwa wafanyabiashara na wananchi katika Soko Kuu la Kariakoo jijini Dar es Salaam. Kampeni hizo zililenga kuongeza uelewa wa jamii kuhusu athari za bidhaa bandia kwa afya, biashara na uchumi wa taifa, pamoja na kuhamasisha wananchi kutoa taarifa kuhusu bidhaa zinazotiliwa shaka.
Maadhimisho hayo yamefanyika chini ya kaulimbiu isemayo: “Linda Maisha na Masoko Dhidi ya Pombe, Vilainishi na Sigara Bandia.”

Comments
Post a Comment