SIKU YA MTOTO WA AFRIKA: LHRC YAHIMIZA HAKI, ULINZI NA USALAMA WA WATOTO NCHINI.

 


DAR ES SALAAM

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dkt. Anna Henga, amesema maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika yanapaswa kuwa chachu ya kuimarisha juhudi za kulinda watoto dhidi ya vitendo vya ukatili vinavyoendelea kujitokeza nchini.


Akitoa tamko la LHRC  kwa vyombo vya habari leo jijini Dar es Salaam kuhusu maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika, Dkt. Henga amesema licha ya kaulimbiu ya mwaka huu inayosisitiza upatikanaji wa huduma za maji, usafi wa mazingira na afya kwa kila mtoto, bado watoto wengi wanakabiliwa na changamoto kubwa za usalama zinazotokana na utekaji, mauaji na aina nyingine za ukatili.


Amesema LHRC imepokea kwa masikitiko matukio ya hivi karibuni ya ukatili dhidi ya watoto yaliyotokea katika mikoa ya Tabora, Lindi na Mbeya, ambapo baadhi ya watoto walipoteza maisha huku wengine wakitekwa katika mazingira ya kutatanisha.


Kwa mujibu wa Dkt. Henga, matukio hayo yanaonesha haja ya kuimarisha mifumo ya ulinzi wa mtoto kuanzia ngazi ya familia hadi taifa. Amesisitiza kuwa mamlaka husika zinapaswa kuhakikisha wahusika wa vitendo hivyo wanabainika na kufikishwa mbele ya sheria ili kutoa haki kwa waathirika na kuzuia matukio kama hayo kujirudia.


Aidha, ametoa wito kwa wazazi, walezi, viongozi wa jamii, taasisi za kidini na mashirika ya kiraia kushirikiana katika kuhakikisha watoto wanapata malezi bora na ulinzi stahiki wakati wote.


Dkt. Henga amesema Tanzania ina sheria na mikataba mbalimbali inayolinda haki za watoto, hivyo ni muhimu kuhakikisha utekelezaji wake unakuwa wa vitendo ili kila mtoto aweze kuishi katika mazingira salama na yenye kuheshimu haki zake.

Kichwa herufi kubwa


Amehitimisha kwa kusisitiza kuwa Siku ya Mtoto wa Afrika isiwe tu ya maadhimisho, bali iwe fursa ya kutafakari na kuchukua hatua madhubuti za kuwalinda watoto, ambao ndiyo msingi wa maendeleo ya taifa la baadaye.

Comments

Popular posts from this blog

RC CHALAMILA AWATAKA WENYEVITI NA WATENDAJI KATA NA MITAA DAR KUSIMAMIA ULINZI NA USALAMA.

MAHAFALI YA NANE SHULE YA AWALI NA MSINGI SAI YAFANA, WAZAZI WATAKIWA KULEA WATOTO KATIKA MISINGI YA MAADILI MEMA.