SIKU YA MTOTO WA AFRIKA: WATOTO WAIOMBA SERIKALI KUBORESHA HUDUMA ZA MAJI NA AFYA.
Dar es Salaam.
Watoto nchini wameiomba Serikali kuongeza uwekezaji katika huduma za maji safi, usafi wa mazingira na afya ili kuhakikisha wanapata mazingira bora ya kuishi, kujifunza na kukua kwa afya njema.
Wito huo umetolewa leo wakati Tanzania ikiungana na mataifa mengine barani Afrika kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika, ambayo mwaka huu imebeba kaulimbiu ya “Kuhakikisha Upatikanaji wa Huduma za Maji, Usafi wa Mazingira na Afya kwa Kila Mtoto Barani Afrika.”
Mmoja wa watoto walioshiriki katika maadhimisho hayo, Noreen Martin, amesema watoto wenye ulemavu hukumbana na changamoto kubwa pale vyoo vinapokosa maji au miundombinu ya usafi inapokosa kuzingatia mahitaji yao, jambo linaloathiri afya na ustawi wao.
Kwa upande wake, Mahri Yusuf amesema kuwekeza katika maji safi, usafi wa mazingira na afya ni kuwekeza katika kutimiza ndoto za watoto wa Afrika, akieleza kuwa huduma hizo ni msingi wa elimu bora, afya njema na maendeleo ya watoto.
Hata hivyo akitoa tamko kuhusu maadhimisho hayo Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Dkt. Anna Henga, ameitaka Serikali kutenga bajeti ya kutosha kwa ajili ya kuboresha huduma za maji safi na salama, hasa katika maeneo ya vijijini na mashuleni, akisema uwekezaji katika sekta ya maji, usafi wa mazingira na afya ni muhimu katika kulinda haki za watoto na kuimarisha ustawi wao.
Tamko hilo limetolewa na zaidi ya watoto 40 waliokutanishwa na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) kwa kwa kushirikiana na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), wakisisitiza umuhimu wa kuhakikisha kila mtoto anapata huduma stahiki bila kubaguliwa.

Comments
Post a Comment