TAMWA YATEMBELEA SHULE YA SEKONDARI MUGABE, YAHIMIZA ULINZI WA HAKI ZA WATOTO.
Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) kimetembelea Shule ya Sekondari Mugabe jijini Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika, ambapo kimetoa wito kwa jamii kuimarisha ulinzi wa haki na usalama wa watoto.
Wakati wa ziara hiyo, TAMWA ilikutana na walimu pamoja na wanafunzi wa shule hiyo kwa lengo la kutoa elimu kuhusu haki za watoto, wajibu wao na namna ya kujilinda dhidi ya vitendo vya ukatili vinavyoweza kuathiri ustawi wao.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Dkt. Rose Reuben, amesema watoto ni msingi muhimu wa maendeleo ya taifa na hivyo wanapaswa kulindwa, kulelewa katika mazingira salama na kupewa fursa sawa za kielimu na kijamii.
Amesema jukumu la kuwalinda watoto ni la jamii nzima, likiwemo la wazazi, walimu na viongozi wa jamii kuhakikisha kila mtoto anapata malezi bora na haki zake zinazingatiwa.
Wakizungumza kwa niaba ya wanafunzi wenzao, Samia Kassim na Abdallah Shabani wameishukuru TAMWA kwa elimu waliyoipata, wakisema imewasaidia kuelewa kwa undani haki zao na namna ya kujilinda.
Kwa upande wake, mwalimu Annamaria amesema elimu ya haki za watoto ni muhimu kwani inawasaidia wanafunzi kujitambua na kuchukua tahadhari dhidi ya vitendo vya ukatili.
Hata hivyo Katika ziara hiyo TAMWA ilitoa zawadi mbalimbali kwa wanafunzi, pia wanafunzi walipata nafasi ya kujifunza kuhusu haki na wajibu wao,pamoja na kushiriki mijadala iliyowasaidia kuongeza uelewa kuhusu masuala ya haki,wajibu na ulinzi wa mtoto.




Comments
Post a Comment