TFS YAENDELEA KUIMARISHA USTAWI WA WATUMISHI KUPITIA ELIMU YA AFYA YA AKILI, VVU NA MAGONJWA SUGU YASIYOAMBUKIZA



Na Mwandishi Wetu, Dodoma


Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) umeendelea kutekeleza juhudi za Serikali za kuimarisha afya na ustawi wa watumishi wa umma kwa kutoa mafunzo kuhusu udhibiti wa VVU na UKIMWI, magonjwa sugu yasiyoambukiza, afya ya akili na dhana ya ujumuishaji wa anuai za jamii mahali pa kazi.


Mafunzo hayo yaliyofanyika leo Juni 06,2026 katika Ukumbi wa Mesuma jijini Dodoma yalifunguliwa na Naibu Kamishna wa Uhifadhi anayesimamia Huduma Saidizi na Utawala wa TFS, DCC Emmanuel Kiboko, na kuwashirikisha jumla ya wahifadhi 116 kutoka Makao Makuu ya TFS na ofisi mbalimbali za Kanda ya Kati.


Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, DCC Kiboko alisema Serikali imeweka miongozo mbalimbali inayolenga kuimarisha ustawi wa watumishi wa umma, ikiwemo Mwongozo wa Kudhibiti VVU na UKIMWI Mahali pa Kazi, hivyo taasisi zinapaswa kuendelea kutoa elimu na kuhamasisha watumishi kujali afya zao.


Alisema afya ya akili imeendelea kuwa moja ya masuala muhimu yanayohitaji kupewa kipaumbele katika maeneo ya kazi kutokana na mchango wake katika ustawi wa watumishi na ubora wa huduma zinazotolewa kwa wananchi.


“Ni muhimu kwa watumishi kuelewa changamoto mbalimbali zinazoweza kuathiri afya ya akili na namna ya kukabiliana nazo. Elimu hii inasaidia kujenga mazingira bora ya kazi na kuimarisha mahusiano mahali pa kazi,” alisema DCC Kiboko.


Aliongeza kuwa mafunzo hayo yanatoa fursa kwa watumishi kupata uelewa kuhusu vihatarishi vya afya ya akili, mbinu za kudhibiti msongo wa mawazo pamoja na umuhimu wa kupata ushauri wa kitaalamu pale inapobidi.


DCC Kiboko alibainisha kuwa mazingira ya kazi na changamoto za kijamii zinazowakabili watumishi zinaweza kuwa chanzo cha msongo wa mawazo, hivyo ni muhimu kwa taasisi kuendelea kuwekeza katika elimu na mifumo ya usaidizi inayolenga kulinda afya ya akili ya watumishi.


Kwa upande wake, Daktari Hafidh Amir kutoka Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) aliwahamasisha watumishi kujitokeza kupima VVU na magonjwa sugu yasiyoambukiza ili kufahamu hali zao za afya na kupata huduma mapema pale inapohitajika.


Alisema TACAIDS imeendelea kusogeza huduma karibu na wananchi na watumishi wa umma kupitia maeneo ya kazi na mikutano mbalimbali ili kuongeza upatikanaji wa huduma za kinga, upimaji na ushauri nasaha.


“Tunawahimiza watumishi kutumia fursa hizi muhimu za kupima afya zao. Utambuzi wa mapema ni hatua muhimu katika kinga na matibabu ya magonjwa mbalimbali,” alisema Dk. Amir.


Awali, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi na Meneja wa Rasilimali Watu wa TFS, SACC Bahati Mtomaye, alisema mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa Mwongozo wa Serikali wa Kudhibiti VVU, UKIMWI na Magonjwa Sugu Yasiyoambukiza Mahali pa Kazi wa mwaka 2014.


Alifafanua kuwa mafunzo hayo yanalenga kuimarisha afya za watumishi, kuongeza uelewa kuhusu afya ya akili, kudhibiti msongo wa mawazo na kuhamasisha mazingira jumuishi yanayowezesha kila mtumishi kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.


“TFS inaendelea kutambua kuwa rasilimali watu ndiyo msingi wa mafanikio ya taasisi. Hivyo, uwekezaji katika afya, ustawi na maendeleo ya watumishi ni sehemu muhimu ya kuhakikisha huduma bora zinaendelea kutolewa kwa wananchi,” alisema Mtomaye.


Kupitia mafunzo hayo, washiriki walipata elimu kuhusu kinga na udhibiti wa VVU na UKIMWI, magonjwa sugu yasiyoambukiza, afya ya akili, usimamizi wa msongo wa mawazo pamoja na umuhimu wa kujenga mazingira ya kazi yenye ushirikiano, heshima na ujumuishaji kwa watumishi wote.


Mafunzo hayo ni sehemu ya mkakati mpana wa TFS wa kuimarisha ustawi wa watumishi I’m wake, kutambua mchango wao katika uhifadhi na usimamizi endelevu wa rasilimali za misitu na nyuki, na kuhakikisha taasisi inaendelea kuwa na nguvu kazi yenye afya, tija na uwezo wa kutoa huduma bora kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.



Comments

Popular posts from this blog

RC CHALAMILA AWATAKA WENYEVITI NA WATENDAJI KATA NA MITAA DAR KUSIMAMIA ULINZI NA USALAMA.

MAHAFALI YA NANE SHULE YA AWALI NA MSINGI SAI YAFANA, WAZAZI WATAKIWA KULEA WATOTO KATIKA MISINGI YA MAADILI MEMA.