WADAU WAHAMASISHWA KUSHIRIKI JUKWAA LA MWAKA LA MASHIRIKA YASIYO YA KISERIKALI 2026


DAR ES SALAAM – Zaidi ya washiriki 3,000 kutoka Tanzania na nchi za Afrika Mashariki wanatarajiwa kushiriki Jukwaa la Mwaka la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGOs) 2026, litakalofanyika Oktoba 20 hadi 22 katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete (JNICC) jijini Dodoma.


Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NaCoNGO), Jasper Makala, ametoa wito kwa mashirika yasiyo ya kiserikali, taasisi za Serikali, sekta binafsi, washirika wa maendeleo na wananchi kushiriki kikamilifu katika maandalizi na utekelezaji wa jukwaa hilo muhimu kwa maendeleo ya taifa.


Makala amesema jukwaa la mwaka huu litafanyika chini ya kaulimbiu ya “Fikra Mpya Kuhusu Uendelevu wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali: Ubunifu, Ubia na Upatikanaji wa Rasilimali Fedha Kupitia Vyanzo vya Ndani,” ikilenga kuhamasisha sekta hiyo kuimarisha uwezo wa kujitegemea na kuongeza mchango wake katika maendeleo ya jamii.


Amesema jukwaa hilo litatumika kujadili mikakati ya kupunguza utegemezi wa ufadhili wa nje kwa kuimarisha vyanzo vya ndani vya rasilimali, kukuza ushirikiano baina ya wadau na kuhimiza matumizi ya teknolojia na ubunifu katika utekelezaji wa shughuli za maendeleo.


Kwa mujibu wa Makala, jukwaa hilo pia litakuwa fursa ya kujadili mafanikio, changamoto na fursa zilizopo katika sekta ya mashirika yasiyo ya kiserikali, huku likiweka mazingira ya kubadilishana uzoefu na kujenga ushirikiano wenye tija kwa maendeleo ya nchi.


Amebainisha kuwa kabla ya jukwaa la kitaifa kufanyika, kutakuwa na majukwaa ya ngazi ya wilaya yatakayofanyika Juni na Julai, pamoja na majukwaa ya ngazi ya mikoa yatakayofanyika Agosti na Septemba mwaka huu kwa lengo la kukusanya maoni na mapendekezo kutoka kwa wadau wa maendeleo.


Makala amesisitiza kuwa mashirika yasiyo ya kiserikali yanaendelea kuwa wadau muhimu katika sekta mbalimbali zikiwemo elimu, afya, jinsia, uwezeshaji wa wanawake na vijana, utawala bora pamoja na maendeleo ya jamii, hivyo ushiriki mpana wa wadau utachangia kuimarisha mchango wa sekta hiyo katika kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.


Jukwaa la Mwaka la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali huandaliwa na NaCoNGO kwa kushirikiana na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum pamoja na wadau wengine wa maendeleo.


Comments

Popular posts from this blog

RC CHALAMILA AWATAKA WENYEVITI NA WATENDAJI KATA NA MITAA DAR KUSIMAMIA ULINZI NA USALAMA.

MAHAFALI YA NANE SHULE YA AWALI NA MSINGI SAI YAFANA, WAZAZI WATAKIWA KULEA WATOTO KATIKA MISINGI YA MAADILI MEMA.