WATAALAMU WA MAABARA WATAKIWA KUIMARISHA USALAMA WA UTUNZAJI WA VIMELEA HATARISHI NA SAMPULI ZA MUDA MREFU.
Arusha
Wataalamu wa maabara nchini wametakiwa kuzingatia kwa umakini mkubwa maadili na viapo vya taaluma yao ili kuhakikisha jamii inalindwa dhidi ya majanga yanayoweza kusababishwa na utunzaji usio salama wa vimelea hatarishi pamoja na sampuli zinazohifadhiwa kwa muda mrefu.
Wito huo umetolewa na Mratibu wa Afya Moja kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Bi. Valentino Sanga, wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha siku tano kinachofanyika jijini Arusha kuanzia Juni 15 hadi 19, 2026.
Akizungumza katika ufunguzi huo, Bi. Sanga amesema kuwa kikao hicho kinalenga kuwajengea washiriki uwezo kupitia kubadilishana uzoefu, kukumbushana wajibu wao wa kitaaluma na kujifunza maarifa mapya yanayozingatia miongozo ya kisasa ya kitaifa na kimataifa kuhusu usalama wa maabara.
Amesisitiza kuwa wataalamu wanapaswa kutumia kikao hicho kama fursa ya kuboresha utendaji wao, hususan katika kuzuia na kubaini mapema vihatarishi vya kiafya, pamoja na kuhakikisha vimelea hatarishi na sampuli zinazohifadhiwa kwa muda mrefu zinatunzwa kwa usalama ili zisije zikawa chanzo cha madhara kwa jamii.
"Tukitumia kikao hiki vizuri, tutaweza kuimarisha mifumo ya kinga, utambuzi wa mapema wa vihatarishi na usimamizi salama wa vimelea na sampuli zinazohifadhiwa kwa muda mrefu ili kuzuia madhara kwa jamii," amesema Bi. Sanga.
Aidha, amefafanua kuwa wataalamu hao wanapaswa kuzingatia kikamilifu maadili ya taaluma yao, akibainisha kuwa uzembe katika utunzaji wa vimelea unaweza kusababisha madhara makubwa kwa wananchi na kuwa kinyume na dhamira ya kazi waliyopewa.
Pia amewahimiza washiriki kuendelea kuzingatia miongozo ya kitaifa na kimataifa inayosimamia usalama wa maabara, akisisitiza kuwa Tanzania ni sehemu ya mikataba mbalimbali ya kimataifa inayolenga kulinda afya na usalama wa jamii kupitia utekelezaji wa viwango vinavyokubalika kimataifa.
Kwa upande wake, mdau wa maendeleo kutoka taasisi ya Center for International Health, Education and Biosecurity Tanzania (CIHEB-Tanzania), Bw. Samwel Mulungu, amesema taasisi hiyo kupitia Mradi wa Usalama wa Afya Duniani (Global Health Security – GHS) imeunga mkono mafunzo hayo ili kujenga uelewa wa pamoja miongoni mwa wataalamu kuhusu namna bora ya kudhibiti na kuhifadhi vimelea hatarishi.
Amefafanua kuwa vimelea vinavyohifadhiwa maabara ni suala nyeti linalohitaji umakini mkubwa, kwani hitilafu katika utunzaji wake inaweza kuhatarisha si wataalamu pekee bali pia jamii kwa ujumla kutokana na uwezekano wa kusambaa kwa maambukizi.
"Utunzaji usiozingatia taratibu za kitaaluma unaweza kusababisha madhara makubwa kwa afya ya umma. Historia imewahi kushuhudia athari za baadhi ya vimelea hatarishi, ikiwemo kimeta, pale mifumo ya usalama inapokuwa dhaifu," amesema Bw. Mulungu.
Jumla ya wataalamu 26 kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Afya, Maabara ya Taifa, vituo vinavyohifadhi vimelea na sampuli, hospitali za mikoa, kanda na taifa, pamoja na vyuo na taasisi mbalimbali za Serikali, wanashiriki katika mafunzo hayo yanayolenga kuimarisha usalama wa maabara na ulinzi wa afya ya jamii.

Comments
Post a Comment